Mahakama ya Wilaya ya Newala imeadhimisha siku ya sheria nchini siku ya Jumatano tarehe 06/02/2019 katika viwanja vya mahakama ya Wilaya ya Newala kwa kuwakumbusha wadau wa mahakama kutimiza wajibu wao kwa kufuata maadili ili wananchi waweze kupata haki zao.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na wageni mbalimbali wakiwemo mahakimu wa ngazi mbalimbali wa mahakama ya mwanzo, watumishi wa idara za ofisi za serikali, mashirika ya umma na asasi zisizo za kiserikali, viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa na wananchi.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, kwa niaba ya hakimu mkazi wa Wilaya ya Newala, Bi. Devotha Salum amesisitiza kuwa wadau hao ambao ni Polisi, Magereza, Bunge, taasisi ya kupambana na kuzuia rushwa, wadhamini, ofisi zote za serikali, wazee wa baraza na mawakili wa kujitegemea wanatakiwa kuwa watii wa sheria, waaminifu, wavumilivu na waelewa wa tabia za watu, wanaopenda ukweli na uwazi, na wanaopenda kujifunza na kubadilika ili waweze kutoa huduma na haki kwa wananchi.
Akiendelea kuzungumza na wananchi, Bi.Devotha ameeeleza kuwa wajibu wa mahakama ni kutoa na kusimamia haki kwa kufuata misingi ya sheria na hasa katika dhana nzima ya mgawanyiko wa madaraka na kuwa Mahakama ni lazima iwe huru katika kutoa maamuzi yake bila kuingiliwa na mihimili mingine.
Siku ya sheria nchini huadhimishwa kila mwaka na ni maalum kwa kutoa elimu kwa umma na pia kukumbushana wajibu, kujikosoa na kuwa tayari kukosolewa kwa dhamira moja ya kuwatumikia wananchi ili kuhakikisha haki inapatikana.
Katika maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Mussa Chimae alipata nafasi ya kuzungumza ambapo aliwataka wananchi wa Newala kumrudia Mungu na kukemea tabia ya vijana kuwapa ujauzito wanafunzi na kupelekea watoto hao kukatiza masomo yao hivyo kuua ndoto na malengo yao.
'Newala tubadilike, taarifa za mimba kwa wanafunzi ni nyingi. Watoto wana haki ya msingi ya kupata elimu, tuwaache wasome, tuwasimamie kama wazazi. Leo ni siku ya haki hivyo iwe vuguvugu la kuanzisha utoaji wa haki kwa watoto. Sisi ni wadau hivyo tushirikiane kuufichua uovu huu na kutoa ushahidi' alisisitiza Bw. Chimae.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya sheria nchini kwa mwaka 2019 ni 'UTOAJI WA HAKI KWA WAKATI: WAJIBU WA MAHAKAMA NA WADAU'.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa