Maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani katika Mkoa wa Mtwara leo tarehe 01/05/2021 yamefanyika katika kiwanja cha shule ya msingi Amani iliyopo katika Wilaya ya Tandahimba.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Mhe. Sebastian Waryuba, Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa.
Katika maadhimisho hayo, Mhe. Waryuba amewataka watumishi kuwajibika vyema katika kazi zao ili maslahi bora wanayoyadai yaendane na utendaji wao wa kazi, kama kauli mbiu ya siku ya wafanyakazi duniani kwa nchi ya Tanzania mwaka huu 2021 inavyosema "Maslahi bora, mishahara juu. Kazi iendelee."
Sherehe za madhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani Mkoa wa Mtwara zimeenda sambamba na kuwatambua wafanyakazi bora wa Ofisi za Mikoa, Halmashauri, Taasisi za Serikali na mashirika ya umma ambapo walipatiwa vyeti vya kuwatambua na zawadi ikiwa ni hamasa ya wafanyakazi hao na wengine kufanya vizuri zaidi katika majukumu yao maeneo yao ya kazi.
Watumishi bora wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala kwa mwaka 2021, wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kukabidhiwa vyeti vyao vya pongezi pamoja na zawadi kwenye maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani, Mkoa wa Mtwara.
Kwa Halmashauri ya Wilaya ya Newala jumla ya watumishi bora 16 kutoka idara za Utumishi na Utawala, Fedha, Kilimo, Afya, Maendeleo ya jamii, Ujenzi, Mifugo, Elimu Msingi na Elimu Sekondari walitambuliwa na kupatiwa vyeti na zawadi.
Sherehe ya maadhimisho hayo ilihudhuriwa na wakuu wa wilaya za mkoa wa Mtwara; makatibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara; Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya na Miji, Wenyeviti wa Halmashauri zote za mkoa wa Mtwara; viongozi wa vyama vya wafanyakazi; wakuu wa taasisi na mashirika, watumishi, waandishi wa habari na wananchi.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa