Pichani ni Waziri wa Maji Prof. Makame Mbarawa (wa mbele katikati aliyevaa kofia), Mkuu wa Wilaya ya Newala Mhe. Aziza Mangosongo (wa mbele kulia) na Mhandisi wa Maji Wilaya Eng. Nsajigwa Sadiki, wakielekea kukagua mitambo ya Maji kwenye chanzo cha Maji Mitema, mara baada ya Prof. Mbarawa Kuwasili kwenye chanzo hicho tarehe 18/10/2019.
Wananchi wa maeneo ya jirani na vyanzo vya maji Wilayani Newala, wametakiwa kuvitunza na kuviendeleza vyanzo vya maji vilivyopo katika maeneo yao.
Akitoa wito huo kwa wananchi wa kijiji cha Mitema Wilayani Newala tarehe 18 octoba,2018 alipokuwa katika Ziara yake ya kukagua vyanzo vya maji na kusikiliza kero za wananchi kuhusiana na maji, Waziri wa Maji Mhe Prof. Makame Mbarawa, amesema vyanzo vya maji vilivyopo katika maeneo yetu ni muhimu sana, kwani vimekuwepo tangu miaka mingi na kutunzwa na watu mbalimbali hadi kufikia hapa, hivyo hakuna budi kwa kila mwananchi kuendelea kuvitunza na kuvilinda, ili viweze kuisadia jamii na watanzania wote kiujumla, na hasa kizazi kijicho.
Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa akiwa katika kijiji cha Makukwe kilichopo Kata ya Makukwe Wilayani Newala, aliweza kutatua kero kubwa ya ugawaji maji kwa wananchi, ambapo wananchi walilalamikia wahusika wa maji kwa kuwauzia nusu ndoo kila siku ikiwa na maana ya ndoo moja, hali iliyowafanya wakose uhuru wa kutumia maji hayo ipasavyo.
Kufuatia hilo, ndipo Prof. Mbarawa kama Waziri mwenye Dhamana, alipoamua kuagiza mabadiliko yafanyike na kwamba kila mwananchi anapaswa kujaziwa ndoo yake mpaka juu, ili kuepukana na muendelezo wa shida ya maji mara kwa mara, na kuepusha migogoro ya maji kwa wananchi wa Makukwe, jambo ambalo kwa hakika, liligusa hisia za wananchi hao na kuonyesha wazi kuridhishwa na ujio wa Waziri wa Maji. “Kuanzia leo, nataka kila mwananchi anapochotewa maji, ndoo ijazwe mpaka hapa juu, sitaki kusikia tena lalamiko kama hili” Alisema Prof. Mbarawa mbele ya wananchi wa Makukwe huku akionyesha mfano wa ujazo wa maji katika ndoo unavyopaswa kuwa.
Nae Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Eng: Nsajigwa P. Sadiki, alitoa taarifa ya mradi huo wa Maji Makukwe, ambao uliibuliwa na wananchi wa kijiji cha Makukwe kwenye Mkutano Mkuu wa kijiji hicho uliofanyika mwaka 2010, na kwamba mradi huo, ni miongoni mwa miradi mitatu ya maji ambayo inatekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Newala, kupitia Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Maarufu kama mradi wa vijiji 10).
Waziri wa Maji Mhe. Prof. Makame Mbarawa (wa kwanza kushoto) akipewa maelezo ya mitambo ya mradi wa maji alipokuwa kwenye chanzo cha Maji kijiji cha Mitema Wilayani Newala, tarehe 18/10/2019.
Mradi huo wa Maji Makukwe unaogharimu zaidi ya Shilingi bilioni 4.9, una lengo la kuwanufaisha wananchi wapatao 28,703 wa vijiji vya Makukwe, Mtunguru, Mkwedu, Kilidu, Machenje, Lengo, Ngalu, Mandala, Namkonda, Mnauja, Chiuta, Matale, Mchedebwa, Songambele, Mpwapwa, Mchemo A, Mchemo B, Mkupete, Chiule, Mango na Mitema, na unatarajiwa kukamilika baada ya miezi sita.
Hii ni mara ya pili kwa Waziri wa Maji Prof. Makame Mbarawa, kutembelea Miradi ya Maji ya Halmashauri ya Wilaya ya Newala, kwa lengo la kusimamia utekelezaji wa mipango ya Serikali ya Awamu ya Tano, ya kuwahudumia watanzania.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa