Wanafunzi wote wa shule za msingi na sekondari Wilayani Newala, wameaswa kutotumia mwanya wa kupata chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi, kuendeleza vitendo vya ngono, wakiamini kwamba tayari wanayo kinga ya ugonjwa hatari na hivyo wapo huru kutumika watakavyo.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Newala Mhe. Aziza Mangosongo, alipokuwa akizindua rasmi chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi, uzinduzi uliofanyika tarehe 25/04/2018 katika shule ya sekondari Mpotola, iliyopo Wilaya ya Newala Mkoani Mtwara.
Mhe. Mangosongo amesema chanjo hiyo inahusisha watoto wakike wenye umri wa miaka 14, ambao kimsingi wengi wao bado ni wanafunzi na ni taifa la kesho, hivyo haina sababu kwa wao kutumia kigezo cha kupata chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi, kiwe ruksa ya kuwa huru kuendeleza tabia mbaya ya kufanya ngono wakiwa masomoni, na hivyo wajiepushe kabisa na vitendo vya ngono, kwani kufanya hivyo kunaweza kuhatarisha maisha yao ya sasa na ya baadae, ikiwa ni pamoja na kukatisha ndoto zao.
Katika uzinduzi huo, Mhe. Mangosongo pia ameishukuru serikali ya awamu ya tano chini ya Wizara ya afya,maendeleo ya jamii jinsia na watoto kwa kuliona hili na kutoa chanjo kwa watoto, na kwa kufanya hivyo, serikali itaokoa maisha ya ya watanzania wengi, kwani utafiti unaonyesha zaidi ya 30% ya vifo vitokanavyo na saratani kwa wanawake, vinasababishwa na saratani ya mlango wa kizazi, ikifuatiwa na saratani ya matiti.
Aidha lengo la serikali kuanzisha chanjo hii, ni kupunguza vifo vitokanavyo na saratani, kupunguza gharama za matibabu kwani inakisiwa kuwa kumtibu mgonjwa mmoja mwenye saratani,ni shilingi milioni 5.5 ukiacha gharama nyingine za uchunguzi, wakati kupata chanjo moja itakayomkinga mtu na saratani ya mlango wa kizazi ni shilingi elfu 30 tu.
Katika hafla hiyo ya uzinduzi wa chanjo iliyoambatana na siku ya malaria Duniani, halmashauri ya Wilaya ya Newala kupitia idara ya afya, imefanya zoezi la upimaji wa ugonjwa wa malaria, ambapo jumla ya watu 198 waliokuwepo kwenye hafla hiyo waliweza kupimwa malaria, na 61 kati yao, vipimo vimeonyesha kuwa wana na ugonjwa wa malaria na hivyo wamepatiwa dawa za kutibu malaria, na wakati huo huo pia watu 24 wameweza kupewa chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi, watoto 8 wamepata chanjo ya polio ya matone matatu, watoto 8 pia wamepata chanjo ya polio sindano na mtoto mmoja tu amepata chanjo ya polio matone ama polio zero kwa lugha ya kitaalamu.
Kauli mbiu ya siku ya malaria Duniani mwaka huu wa 2018 ni
“Mimi nipo tayari kutokomeza malaria Tanzania, wewe je?”
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa