Maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani kwa Mkoa wa Mtwara yamefanyika siku ya Jumatano tarehe 01/05/2019 katika Wilaya ya Masasi mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Gelasius Byakanwa.
Katika risala ya wafanyakazi kwa mgeni rasmi, wafanyakazi waliiomba Serikali kupitia viwango vya mishahara ya wafanyakazi wa umma na sekta binafsi na kuja na viwango vipya kwa kuwa viwango vilivyopo sasa havikidhi mahitaji ukilinganisha na kupanda kwa gharama halisi za maisha za sasa; waliipongeza Serikali kwa kulipa madeni yanayotokana na mishahara, likizo, uhamisho, matibabu na masomo na kuondoa au kupunguza madeni ya watumishi yasiyokuwa ya lazima. Hata hivyo waliomba madeni yaliyohakikiwa yalipwe ili kuongeza morali ya kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.
Pia watumishi waliendelea kuiomba Serikali kuwapandisha madaraja kwa wakati na kurekebishiwa mishahara yao kulingana na madaraja mapya waliyonayo; kuwekwa kwa mazingira yanayovutia ya uwekezaji wa viwanda vidogo vidogo ili kuwapa wananchi fursa ya kupata ajira; na Serikali kuongeza idadi ya wafanyakazi kwenye vituo vipya vya afya na hospitali za wilaya ili kuboresha zaidi huduma za afya.
Akizungumza na wafanyakazi, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara amewataka wafanyakazi kuwa na umoja unaosimamia maslahi yao kwa kutumia utaratibu mzuri wa kuwasilisha madai yao kwa Serikali kwa kuwa Serikali ni sikivu na inajali maslahi ya wafanyakazi na imejipanga kuyaboresha maslahi ya wafanyakazi kadri uchumi unavyoimarika.
Amewaeleza wafanyakazi kuwa, kama kauli mbiu ya siku ya wafanyakazi mwaka huu 2019, nchi haiwezi kufika katika uchumi wa viwanda na wa kati kama hawapo wafanyakazi wenye maslahi bora na amewahakikishia wafanyakazi kuwa maombi na mawazo yao yote yamechukuliwa na yatafanyiwa kazi.
Mei Mosi ilianza karne ya 19, wakati mapinduzi ya viwanda yanashika hatamu katika Bara la Ulaya. Kutokana na uchache wa wafanyakazi na tamaa ya waajiri kwa wakati ule kutaka kuzalisha zaidi na kwa faida zaidi wafanyakazi walifanyishwa kazi zaidi ya masaa 18 kwa siku mfululizo na ujira mdogo. Baada ya wafanyakazi kuchoshwa na hali ile walianzisha vuguvugu la mapinduzi kujinusuru na ukandamizaji wa waajiri wakishinikiza saa za kazi zipunguzwe kufikia 8 na ujira uongezwe.
Aidha walidai uhuru wa kuanzisha umoja wao ili wapate siku ya kujadili changamoto wanazokumbana nazo katika kipindi cha mwaka mzima. Siku waliyokubaliana ni tarehe 01 Mei kila mwaka. Hii ndiyo ikawa mwanzo wa siku ya Mei Mosi duniani.
Sherehe hizi huambatana na kauli mbiu ya kila mwaka ikiwa ni tamko mahususi la wafanyakazi kitaifa. Kauli mbiu ya siku ya wafanyakazi kwa mwaka 2019 ni ‘Tanzania ya Uchumi wa Kati inawezekana, wakati wa Mishahara na Maslahi bora kwa wafanyakazi ni sasa’.
Kwa Mkoa wa Mtwara, maadhimisho hayo yalihudhuriwa na Mkuu wa mkoa wa Mtwara, wakuu wa wilaya, wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa mkoa, wenyeviti wa Halmashauri za wilaya,na miji, wataalamu wa Sekretariet ya mkoa, makatibu tawala wa wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri za wilaya, miji na manispaa, wakuu wa taasisi za umma Mkoa wa Mtwara, wenyeviti wa vyama vya wafanyakazi na mwenyekiti wa CCM wilaya ya Masasi.
Siku ya Wafanyakazi duniani kwa Tanzania, kitaifa iliadhimisha katika Mkoa wa Mbeya na kwa Mkoa wa Mtwara kimkoa maadhimisho yalifanyika katika viwanja vya Boma Wilaya ya Masasi.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa