Mkuu wa Wilaya ya Newala Mhe. Aziza Mangosongo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa jana tarehe 12/02/2021 amezindua zoezi la upandaji wa miti kwa Mkoa wa Mtwara katika eneo la shule ya sekondari Mpelepele iliyopo katika kijiji cha Mdimba Mpelepele Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Mkuu wa Wilaya ya Newala Mhe. Aziza Mangosongo akizungumza katika uzinduzi wa upandaji wa miti kwa Mkoa wa Mtwara katika shule ya sekondari Mpelepele
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mhe. Mangosongo kuwa upandaji wa miti katika maeneo yetu una faida kubwa.
"miti ni chanzo cha chakula, ni malighafi pia ni chanzo cha hewa safi. Nitumie fursa hii kuwataka wa Mtwara kupanda miti na kuitunza." alisema Mhe. Mangosongo.
Mhe. Mangosongo pia ametoa wito kwa Halmashauri zote za Mkoa wa Mtwara kuandaa programu za kupanda miti na kuitunza, kuongeza bajeti ya mazingira kwa kuandaa vitalu vya miche ya miti na kuigawa bure kwa wananchi na kudhibiti uchomaji moto wa mashamba kwa kuweka sheria ndogo za Halmashauri zinazozuia vitendo hivyo.
"Mkoa wa Mtwara unaendelea kusimamia sheria ya misitu namba 14 ya mwaka 2002 na kanuni zake kwa lengo la kuhakikisha kuwa uharibifu wa misitu unaosababishwa na shughuli za kibinadamu kama vile uvunaji haramu wa misitu, kilimo cha kuhamahama, upanuzi holela wa mashamba ya kilimo, ufugaji holela wa mifugo na uchomaji wa misitu unakomeshwa." Alisema Mhe. Mangosongo.
Akiendelea na uzinduzi huo, Mhe. Mangosongo pia amewaeleza wananchi kuwa sekta hii ni muhimu sana katika ukuaji wa uchumi hasa ukizingatia Taifa lipo katika uchumi wa kati na linatekeleza mkakati wa uchumi wa viwanda.
"Serikali chini ya uongozi wa Mhe. Dokta John Pombe Magufuli imeweka kipaumbele katika swala la kuhifadhi rasilimali za misitu na ufugaji wa nyuki ili sekta hiyo izalishe ajira nyingi zaidi kupitia mazao yake." Alisema Mhe. Mangosongo.
Zoezi hilo la uzinduzi wa upandaji wa miti kwa Mkoa wa Mtwara limehusisha upandaji wa miti 1000 ya mbao na matunda katika eneo la shule ya sekondari Mpelepele na ugawaji wa miche 500 kwa wananchi ili wakapande katika maeneo yao.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa