Timu ya menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Newala pamoja na wawezeshaji 23 jana siku ya Jumatatu tarehe 03/08/2020 wamepatiwa mafunzo elekezi juu ya zoezi la uhakiki wa kaya zilizopo kwenye mpango wa kunusuru kaya masikini unaosimamiwa na TASAF.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bi. Magreth Likonda akifungua mafunzo elekezi ya uhakiki wa walengwa wa mpango wa kunusuru kaya masikini.
Akifungua mafunzo hayo elekezi, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bi. Magreth Likonda amewataka wawezeshaji hao kufuatilia vizuri na kuelewa mafunzo hayo wanayopewa kwa siku mbili na kufanya vizuri kazi hiyo ya uhakiki ambayo kwa sasa taarifa zake zitajazwa moja kwa moja kwenye mfumo wa TASAF na wawezeshaji hao kwa njia ya simu walizopatiwa maalum kwa zoezi hilo.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji TASAF ambaye pia ni mwezeshaji wa mafunzo hayo Bw. Steven Samwel akitoa mafunzo kwa washiriki katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Akitoa ufafanuzi kwenye mafunzo hayo, mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Steven Samwel, amewaeleza washiriki kuwa uhakiki huo utafanyika katika kaya zote za walengwa kwenye kila kijiji ambacho kipo katika mpango wa kunusuru kaya masikini kwa lengo la kupata orodha halisi ya kaya za walengwa wenye vigezo vya kubaki kwenye mpango.
"Uhakiki huu utafanyika kwa njia ya ukaguzi wa vitambulisho vya walengwa vya mpango, vitambulisho vya Taifa na kukusanya taarifa zote za wanakaya walengwa kwa njia ya kielektroniki. " Alisema Bw. Samwel.
Kwa Wilaya ya Newala, uhakiki huo utafanyika katika vijiji 97 vilivyopo kwenye mpango wa kunusuru kaya masikini. Aidha zoezi hili la uhakiki ni hatua ya awali ya kuelekea zoezi la uibuaji wa kaya masikini nyingine ambazo zitaungana na kaya zilizohakikiwa na kukidhi vigezo kupokea ruzuku kutoka TASAF katika kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya TASAF (PSSN II) ambacho kinatarajiwa kufanya utekelezaji wake kwa kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2020 hadi 2023.
Uhakiki wa kaya hizo ambazo tayari zipo kwenye mpango wa kunusuru kaya masikini kwa Wilaya ya Newala unatarajiwa kufanyika kwa siku tatu kuanzia Jumatano tarehe 05/08/2020 hadi Ijumaa tarehe 07/08/2020.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa