Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa mwaka 2018 Ndugu Charles Francis Kabeho, ameridhishwa na hali ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Newala kwa kusema kuwa, thamani ya pesa iliyotolewa na serikali kwa miradi hiyo inalingana na ubora wa miradi iliyotekelezwa.
Hayo yamejiri wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, uliokimbizwa Wilayani Newala tarehe 15/06/2018 katika Vijiji 21, Kata 9 na Tarafa 3 kwa umbali wa Kilomita 102 hadi katika kijiji cha makabidhiano cha Lidumbe Mtoni kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba tarehe 16/06/2018.
Katika miradi yote 7 iliyotembelewa na Mwenge wa Uhuru mwaka 2018, hakuna hata mmoja uliokataliwa kutokana na sababu yoyote, jambo lililopelekea kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Bw. Charles Kabeho kuikubali na kutoa sifa nyingi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Newala, kwa kusema kuwa wao kama wakimbiza Mwenge wa Uhuru 2018, wameridhishwa na kufurahishwa na hali ya utekelezaji wa miradi yote waliyoipitia, kwani imetekelezwa ipasavyo na kwamba thamani ya fedha zilizotolewa na Serikali kwa miradi hiyo, zinalingana kabisa na ubora wa miradi iliyotekelezwa, jambo linalomaanisha utendaji bora na usimamizi mzuri wa fedha za Serikali na wananchi kwa ujumla.
Bwana Kabeho alitumia fursa yake pia kuipongeza halmashauri ya Wilaya ya Newala pamoja na wananchi wake, kwa jitihada kubwa za uwekezaji katika sekta ya elimu kwa kutatua changamoto ya upungufu wa samani uliopo kwenye shule za sekondari kutokana na ongezeko la wanafunzi kufuatia mpango wa elimu bila malipo. Kwani kabla ya jitihada hizi kufanyika, Halmashauri ilikuwa na upungufu wa samani seti 1,119 zikiwemo seti 1,019 za viti na meza kwa ajili ya wanafunzi na seti 100 kwa ajili ya walimu kwenye shule zake zote 15. Mahitaji hayo yametokana na ongezeko la wanafunzi wanaomaliza darasa la saba na kuchaguliwa kujiunga elimu ya sekondari na uwepo wa ongezeko la walimu. Hivyo kwa sasa upatikanaji wa madawati hayo utamaliza tatizo la samani uliopo kwa wanafunzi na walimu, na hii inabeba sura ya kipekee kwa wazazi na wananchi kwa ujumla, ambao wamehusika moja kwa moja katika kuchangia samani hizi, kwani fedha zilizowezesha upatikanaji wa samani hizo, zimetokana na michango ya wananchi kwenye mfuko wao wa Elimu unaochangiwa kupitia makato ya mauzo ya zao la korosho.
Mwenge wa wa Uhuru ukiwa Halmashauri ya Wilaya ya Newala, ulikimbizwa kwenye miradi 7 iliyohusisha uzinduzi wa mradi mmoja (1) wa wapinga rushwa Shule ya Msingi Mtunguru, uwekaji wa mawe ya msingi kwenye miradi mitatu (3) ya vyumba 5 vya madarasa shule ya sekondari Makukwe na ugawaji wa Samani ( Meza na viti) kwa shule za sekondari vyenye thamani ya shilingi milioni 93, kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa nyumba za walimu 6 kwa 1 wa shule ya sekondari Lengo na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa upanuzi wa miundo mbinu ya Kituo cha Afya Kitangari, na kuona miradi mitatu (3) ya Kuona na kukagua Upanuzi wa Miundombinu ya Chuo cha Ualimu Kitangari na onesho la tusome pamoja, Kuona vikundi vya Vijana na Wanawake vya uzalishaji mali kijiji cha Mtopwa na Kuona juhudi za Halmashauri za kupambana na UKIMWI, Madawa ya kulevya, Rushwa na Malaria,ambapo miradi yote 7 ina jumla ya thamani ya shilingi 9,068,608,112/= iliyohusisha pia michango ya wananchi kwa asilimia 0.05%, fedha kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri asilimia 2.79% na ruzuku kutoka Serikali kuu asilimia97.16%.
Kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka huu wa 2018, ni “ELIMU NI UFUNGUO WA MAISHA, WEKEZA SASA KWA MAENDELEO YA TAIFA LETU”
HABARI PICHA ZA MATUKIO MBALIMBALI YA MWENGE WA UHURU MKOANI MTWARA NA WILAYANI NEWALA KWA MWAKA 2018.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe.Gelasius Byakanwa akikabidhiwa Mwenge wa Uhuru kutoka Mkoa wa Ruvuma na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Christina Mndeme, mapokezi hayo kimkoa yalifanyika tarehe 11/06/2018 katika kijiji cha Lumesule Wilayani Nanyumbu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Mussa Chimae akimkabidhi Mwenge wa Uhuru Mkuu wa Wilaya ya Newala Mhe.Aziza Mangosongo mara tu baada ya kuupokea kutoka halmashauri ya mji Newala tarehe 15/06/2018 katika kijiji cha Mkwedu Wilayani Newala.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Ndugu Charles Francis Kabeho akiweka jiwe la msingi katika mradi wa vyumba vitano vya madarasa shule ya sekondari Makukwe Wilayani Newala tarehe 15/06/208.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Ndg. Charles Francis Kabeho akikabidhi samani (viti na meza) za walimu na wanafunzi wa shule za sekondari mara tu baada ya kuweka jiwe la msingi shule ya sekondari Makukwe tar 15/6/2018.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Ndg. Charles Francis Kabeho akizindua mradi wa Klabu ya kupambana na Rushwa shule ta Msingi Mtunguru Wilayani Newala tarehe 15/06/2018, kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Newala Mhe. Aziza Mangosongo.
Jiwe la Msingi la Klabu ya kupambana na Rushwa shule ya msingi Mtunguru.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Ndg. Charles Francis Kabeho akiweka jiwe la msingi katika mradi wa nyumba ya walimu 6 kwa 1 shuke ya sekondari Lengo Wilayani Newala tar 15/6/2018.
Jiwe la msingi katika ujenzi wa nyumba ya walimu 6 kwa 1 shule ya sekondari Lengo.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Ndg. Charles Francis Kabeho akiona kikundi cha uzalishaji mali cha vijana na wanawake wa kijiji cha Mtopwa tarehe 15/06/2018 wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru Wilayani Newala.
Jiwe la msingi la upanuzi wa kituo cha Afya Kitangari.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Ndg. Charles Francis Kabeho akitoa pongezi kwa mradi mzuri wa upanuzi wa miundombinu ya kituo cha Afya Kitangari mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika mradi huo tarehe 15/06/2018.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa