Ofisi ya Rais – Tamisemi imeipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Newala kwa hatua nzuri iliyofikia ya upanuzi wa kituo cha Afya Kitangari na kusema kuwa ujenzi wa miundombinu ya kituo hicho ni mfano wa kuigwa na Halmshauri nyingine hapa nchini.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu – TAMISEMI upande wa Afya Dkt Zainabu Chaula alipokuwa katika ziara yake ya kikazi iliyofanyika tar 6/6/2018 Wilayani Newala, ambapo alitembelea mradi wa upanuzi wa miundombinu ya kituo cha Afya Kitangari, ambao kwa sasa upo katika hatua ya umaliziaji.
Dkt Chaula amesema wameridhishwa na kufurahishwa na usimamizi mzuri wa mradi huo na kumpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Mussa Chimae kwa kuhakikisha fedha za wananchi pamoja na serikali zinatumika ipasavyo katika kuboresha huduma za Afya na uzazi salama, na kwamba katika maeneo mbalimbali waliyopita Mkoani Mtwara, Mradi wa kituo cha Afya Kitangari umeonyesha sura ya kipekee inayovutia na inayopaswa kuigwa na Halmashauri nyingine.
Pamoja na kuridhishwa na hali nzuri ya majengo yaliyojengwa katika kituo hicho, pia yapo baadhi ya maeneo machache ambayo Naibu Katibu Mkuu – Tamisemi na kamati yake, wametoa ushauri wa kuyaboresha zaidi na kuongeza baadhi ya vitu, ili kukidhi haja ya upatikanaji huduma pindi huduma hiyo itakapozinduliwa, kwani lengo la serikali ni kuja kuzindua huduma na sio majengo.
Kutokana na hatua nzuri ya upanuzi wa kituo hicho cha Afya Kitangari, Naibu Katibu Mkuu – Tamisemi amesema kuwa serikali ipo tayari kuleta watumishi wa idara ya Afya watakaofanya kazi ya utoaji huduma kwa wananchi watakaofika kutaka huduma katika kituo hicho cha Afya Kitangari na kwamba watumishi hao watafika pindi tu mradi huo utakapokamilika tayari kwa kuanza kutoa huduma.
Nae Mkurugenzi wa Tiba Wizara ya Afya Dkt Dorothy Gwajima, amewapongeza wananchi wa Kitangari kwa kushirikiana kikamilifu na serikali katika kujitolea kuchangia na kuhakikisha miundombinu bora ya Tiba katika kituo hicho, ikiwa ni pamoja na kuwasisitiza wananchi kuendelea kumiliki huduma zitakapoanza, kwani ipo kamati ya usimamizi wa huduma inayoshirikisha wananchi wa Kitangari, ambayo kimsingi ni sera ya serikali inayowataka wananchi kusimamia kikamilifu mipango na huduma inayotolewa, ikiwa ni pamoja na kumshauri Mkurugenzi kwa niaba ya wananchi juu ya utoaji wa huduma ya Afya katika kituo hicho. “Sera imewatengenezea mkakati wa kutengeneza hizi kamati za usimamizi maana ni kituo chenu”Alisisitiza zaidi Dkt Gwajima.
Naibu katibu Mkuu - Tamisemi Dkt Zainabu Chaula (wa katikati) Mkurugenzi wa USAID mradi wa Boresha Afya Dkt Marina Njelekela (wa pili kutoka kushoto), Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Mussa Chimae, pamoja na viongozi wengine walipokuwa wakiongea na wananchi wa Kitangari, mwishoni mwa Ziara ya ukaguzi wa mradi wa kituo cha afya Kitangari, tarehe 6/6/2018.
Ziara ya Naibu Katibu Mkuu – Tamisemi iliyohusu ukaguzi wa mradi wa kituo cha Afya Kitangari unaogharimu jumla ya shilingi milioni 400, iliwahusisha wageni mbalimbali kutoka Tamisemi na Wizara ya Afya, mganga mkuu wa Mkoa wa Mtwara (RMO),Mkurugenzi wa USAID – Boresha Afya Dkt Marina Njelekela, pamoja na viongozi mbalimbali wa sekta na mashirika yanayotoa misaada ya tiba nchini Tanzania.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa