Mkuu wa mkoa wa Mtwara Mhe: Gelasias Byakanwa ameiomba mamlaka ya elimu Tanzania kutoa uhuru wa kubuni ramani ya nyumba za walimu pale wanapotoa msaada wa miradi hiyo.
Mhe Byakanwa ameyasema hayo Wilayani Newala, alipokuwa kwenye ziara yake ya kawaida ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika halmashauri ya Wilaya ya Newala siku ya alhamisi tarehe 19/04/2018, ambapo ameshuhudia ujenzi wa nyumba moja ya kaya sita yaani ( six in one) katika shule ya sekondari Lengo iliyopo Wilaya ya Newala, ambao ulianza tangu mwezi wa pili mwaka huu wa 2018, unaofadhiliwa na mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), na una gharimu jumla ya shilingi milioni 141 ambazo zimetolewa kwa awamu mbili tofauti, awamu ya kwanza ni shilingi milioni 70.5 na awamu ya pili pia ilikuja milioni 70.5 ambazo jumla yake ni milioni 141 zinazotarajiwa kukamilisha nyumba hiyo.
Pichani ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasias Byakanwa (wa kwanza kushoto),Mkuu wa Wilaya ya Newala Mhe. Aziza Mangosongo ( wa pili kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Mussa Chimae (wa tatu kutoka kushoto) na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Mhe. Chitwanga R. Ndembo (anaefuata baada ya Mkurugenzi),wakiwa kwenye mradi wa nyumba ya walimu shule ya sekondari Lengo Wilayani Newala.
Akitoa maoni yake juu ya mradi huo, Mhe Byakanwa amesema mradi wa nyumba inayojengwa katika sekondari hiyo, haitampa uhuru mwanakaya kujitawala na familia yake kulingana na uhalisia wa maisha halisi ya mtanzania, na hivyo Wizara ya Elimu na mamlaka ambazo zinatoa misaada ya nyumba hizo, zitoe na uhuru kwa taasisi husika kudizaini ramani ya nyumba hizo kulingana na mazingira halisi ya eneo husika na familia za walimu hao, kwani kuwepo kwa nyumba hiyo kunatarajiwa kuleta ufanisi mkubwa kwa walimu na wanafunzi wa shule ya sekondari Lengo.
Katika ziara yake Mhe; Byakanwa pia amekagua mradi wa upanuzi wa miundombinu majengo ya kituo cha afya Kitangali, ambapo amewaomba wananchi wa Kitangali kwa kushirikiana na Diwani wao wa kata ya Kitangali, kujitolea kushiriki kujenga wodi ya kina mama au wodi mchanganyiko ambayo itahusisha wagonjwa wa aina zote, kwani kama wananchi hawatashirikishwa kikamilifu na kujitolea kusaidia ujenzi wa miradi kama hiyo, bado itakuwa vigumu kwa serikali kufanya kila kitu na hivyo kuchelewesha huduma na maendeleo kwa ujumla.
Mradi wa upanuzi wa miundombinu majengo ya kituo hicho cha Afya Kitangali unaogharimu jumla ya shilingi milioni 400, unahusisha ujenzi wa nyumba moja ya mtumishi wa kituo hicho na kuboresha huduma za upasuaji, maabara na huduma ya damu salama, chumba cha kuhifadhia maiti, wodi ya wazazi na watoto, kichomea taka, ikiwa ni pamoja na kupunguza vifo na rufaa za kina mama wajawazito ambao walikuwa wanalazimika kukimbizwa hospitali ya mji Newala.
Aidha Mhe Byakanwa ameziomba taasisi zinazotoa misaada ya miradi hiyo, kutoa mgawanyo wa fedha hizo kulingana na eneo husika kwani maeneo kama ya Newala na Mtwara kwa ujumla kuna changamoto ya mabadiliko ya kupanda kwa bei ya vifaa vya ujenzi mara kwa mara, kama saruji na nondo, ikiwa ni pamoja na upatikanaji mgumu wa rasilimali madini kama mchanga, kokoto na mawe, ambavyo vinaongeza ugumu katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Mradi wa kituo cha afya Kitangali ulioanza januari 2018, pamoja na mradi wa ujenzi wa nyumba ya walimu wa shule ya sekondari Lengo, inatarajiwa kukamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu wa 2018.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa