Halmashauri ya Wilaya ya Newala leo tarehe 23/07/2020 imetoa mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu za maji na usafi wa mazingira ngazi ya kaya kwa watendaji wa kata, watendaji wa vijiji na watoa huduma za afya wa kujitolea ngazi ya jamii (WAJA).
Mafunzo hayo ni maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa maji (unawaji wa maji tiririka na sabuni) na usafi wa mazingira (utumiaji wa vyoo bora) katika kaya na vituo vya kutolea huduma ya afya unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, jinsia wazee na watoto.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Bw. Famili Mshaghira akifungua mafunzo ya ukusanyaji takwimu za mradi wa maji na usafi wa mazingira leo tarehe 23/07/2020 katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha walimu Kitangari.
Akifungua mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Famili Mshaghira amewataka washiriki wote kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha.
"Mradi huu ni wa tunapewa pesa kulingana na matokeo tutakayoyapata katika utekelezaji (P4R), hivyo tunatakiwa kuwa makini katika kutekeleza majukumu yetu ili kuleta mafanikio zaidi katika Halmashauri yetu." Alisema Bw. Mshaghira.
Mafunzo hayo yalihusisha kuwapa washiriki uelewa wa pamoja juu ya mradi wa usambazaji wa maji na usafi wa mazingira vijijini, mapokezi na matumizi ya fedha za mradi, viashiria vya matokeo ya mradi ngazi ya kaya na vituo vya kutolea huduma ya afya, ujazaji wa takwimu za maji safi na usafi wa mazingira na utambuzi wa aina za vyoo na sifa zake.
Aidha mpaka sasa Halmashauri ya Wilaya ya Newala imepokea kiasi cha Tsh. 272,830,000 ambapo Tsh. 220,000,000 zitaenda kwenye vituo vya kutolea huduma ya afya vya Kitangari, Mkwedu, Chihangu, zahanati za Mpirani, Maputi, Makukwe, Lengo, Mnali, Mnyeu na Mnyambe na zitatumika kujenga vyoo bora vya wagonjwa na watumishi; kuweka mifumo ya maji tiririka/bomba; kuweka sehemu za kunawia mikono katika maeneo yote muhimu na kuweka bafu katika wodi ya wazazi. Pia Tsh.52,830,000 ni kwa ajili ya shughuli za usimamizi na uboreshaji wa huduma za usafi wa mazingira katika kaya.
Mafunzo hayo yatafanyika kwa siku mbili, siku ya kwanza yatahusisha washiriki kutoka kata 9 na siku ya pili kata 13 watakaowezeshwa kukusanya takwimu za usafi wa mazingira za vijiji vyote, shule na vituo vya kutolea huduma ya afya kwa wakati na kwa usahihi zikiwemo utumiaji wa vyoo bora.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa