Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala jana siku ya Ijumaa tarehe 04/12/2020 wamepiga kura ya kumchagua Mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa Halmashauri yao katika mkutano wa baraza la madiwani uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha walimu Kitangari.
Mkutano huo wa baraza la madiwani ulianza kwa madiwani wateule wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala kula kiapo mbele ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Tandahimba Mhe. Nasra Mkadam Mwinshehe; waheshimiwa madiwani kutoa tamko la maadili mbele ya Afisa Maadili kutoka Sekretariet ya Maadili ya viongozi wa umma kanda ya kusini Mtwara, Bi. Esther Lemther Laizer ili madiwani hao wawe waadilifu katika kuwatumikia wananchi kama walivyoapa.
Diwani mteule wa kata ya Mtunguru, Mhe. Chitwanga Ndembo akila kiapo wakati wa Mkutano wa baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Baada ya viapo hivyo, waheshimiwa madiwani walipata nafasi ya kupiga kura ya kumchagua Mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala ambapo Mhe. Ladda Mfaume Tamimu, diwani wa kata ya Kitangari (CCM) alichaguliwa kuwa mwenyekiti na Mhe. Isabela Dadi Makumbuli, diwani wa kata ya Maputi (CCM) kuwa makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala kwa kura zote za ndiyo kutoka kwa waheshimiwa madiwani 30.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala, Mhe. Ladda Mfaume Tamimu, akiwashukuru waheshimiwa madiwani kwa kumchagua kuwa mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
"Nawashukuru waheshimiwa madiwani wote kwa kuniamini na kunichagua kuwa mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala, Mungu awabariki na tuendelee kushirikiana kuijenga Halmashauri yetu." Alisema Mhe. Lada.
Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala, Mhe. Isabella Dadi Makumbuli akiwashukuru waheshimiwa madiwani kwa kumchagua kuwa makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
"Asanteni kwa kunichagua kuwa makamu mwenyekiti, kikubwa tukafanye kazi kwa ushirikiano tukiamini umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Asanteni sana." Alisema Mhe. Makumbuli.
Aidha pia waheshimiwa madiwani walipata nafasi ya kuunda kamati za kudumu za Halmashauri ya Wilaya ya Newala ambapo zilipatikana kamati nne ambazo tano ambazo ni Kamati ya Elimu, Afya na Maji; Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira; Kamati ya Maadili, Kamati ya Ukimwi; na Kamati ya Fedha.
Baraza hilo la madiwani pia lilipata nafasi ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi, shughuli na maamuzi yaliyofanyika katika kipindi cha mwezi Julai hadi Novemba 2020 katika idara mbalimbali za Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Mkutano huo wa baraza la madiwani umefanyika kwa siku moja na ulihudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Duncan Thebas, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara Bw. Alphayo Kidata, Mkuu wa Wilaya ya Newala Mhe. Aziza Mangosongo, wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Newala, Mhe. Mbunge wa jimbo la Newala vijijini Bi. Maimuna Mtanda, viongozi wa vyama vya siasa vya CCM na ACT wazalendo wilaya ya Newala, viongozi wa dini,maafisa wa Maadili Sekretariet ya Maadili ya viongozi wa umma kanda ya Kusini, Hakimu Mkazi wa wa Wilaya ya Tandahimba Mhe. Nasra Mkadam Mwinshehe, waheshimiwa madiwani, wakuu wa idara na vitengo, wageni waalikwa na waandishi wa habari.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa