Mkuu wa Wilaya ya Newala Mhe. Aziza Mangosongo leo Ijumaa tarehe 07/10/2021 amekabidhi pikipiki 10 kwa vijana wa kikundi cha bodaboda Kitangari Hospitali waliopatiwa pikipiki hizo na Halmashauri ya Wilaya ya Newala ikiwa na mkopo uliotokana na asilimia kumi ya makusanyo ya mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Mmoja wa wanakikundi cha bodaboda cha Kitangari Hospitali akikabidhiwa ufunguo pamoja na kadi ya pikipiki na Mkuu wa Wilaya ya Newala Mhe. Aziza Mangosongo.
"Kila mwaka wa fedha, Halmashauri ya Wilaya ya Newala huwa inatenga asilimia kumi ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kusaidia makundi maalum ya wanawake, vijana na walemavu kwa kutoa mikopo kwa uwiano wa asilimia 4 kwa wanawake, asilimia 4 kwa vijana na asilimia 2 kwa watu wenye walemavu." Alisema Bw. Ally Said, Kaimu Afisa Maendeleo ya jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
"Kwa mwaka wa fedha 2020/2021, mpaka kufikia mwezi Machi 2021, jumla ya Tsh. 76,764,357 zimetolewa kusaidia vikundi hivyo vya wajasiriamali hao kwa uwiano wa asilimia 4, 4, 2 kikiwemo kikundi hiki cha bodaboda kilichopata pikipiki 10 zilizogharimu Tsh. 22,500,000 ambapo pikipiki nane ni aina ya Sinoray, moja Haujue na moja TVS." Alisema Bw. Said.
Kwa sasa Halmashauri ya Wilaya ya Newala inaelekeza nguvu kubwa kwenye kutoa mikopo ya vifaa vitakavyowafanya wanakikundi kuwekeza kwenye utendaji zaidi.
Akikabidhi pikipiki hizo, Mhe. Mangosongo amewataka wanakikundi hao wanaopatiwa pikipiki kuziendesha kwa kufuata sheria za barabarani, na kuhakikisha wanarejesha fedha hizo kwa wakati ili ziingie kwenye mzunguko wa ukopeshaji wa vikundi vingine. Kila aliyepokea pikipiki alizawadiwa na Mhe. Mangosongo lita mbili za petroli kwa ajili ya kuanzia shughuli zao za biashara ya kubeba abiria.
"Nampongeza Mkurugenzi Mtendaji kwa kutenga fedha hizi na kuwakopesha vijana hawa. Umetekeleza Ilani na agizo la Serikali. Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi inasema tuwajali vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kwa kuwapa mikopo itakayowasaidia kuwapandisha kiuchumi. Hongereni sana. " alisema Mhe. Mangosongo.
Akizungumza kwa niaba ya wanakikundi cha bodaboda cha Kitangari Hospitali, Bw. Said Shaban Athumani, katibu wa kikundi hicho aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Newala kwa kuwapatia mikopo hiyo na kuahidi kuwasilisha marejesho ya mkopo wao kwa wakati.
Utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu upo kisheria na Halmashauri ya Wilaya ya Newala mpaka mwezi Machi, 2021 ilitenga Tsh. 79,423,471.74 kwa ajili ya mikopo hiyo.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa