Mkuu wa Wilaya ya Newala Mhe. Aziza Mangosongo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa, jana Jumatatu tarehe 7/12/2020 amefungua rasmi kampeni ya kuondoa mashamba pori na kuongeza uzalishaji kwa wakulima katika kijiji cha Maputi, kata ya Maputi, Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Akizungumza kwenye mkutano na wakulima hao, Mhe. Mangosongo ameeleza kuwa kampeni hiyo ina manufaa makubwa sana kwa kuwa itaongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali katika maeneo yetu kwa kuwawezesha wakulima kuondoa mashamba pori yote kwa kuyasafisha, kulima na kupanda mazao mbalimbali.
Kulingana na taarifa za uzalishaji wa zao la korosho zilizotolewa na Chama Kikuu cha Ushirika cha Newala na Tandahimba (TANECU), taarifa inaonyesha uzalishaji wa zao la korosho umeanza kushuka.Takwimu za uzalishaji zinaonyesha kuwa, mwaka 2015/2016 uzalishaji wa korosho ulikuwa tani 60,000; mwaka 2016/2017 tani 98,000; mwaka 2017/2018 tani 106,000; mwaka 2018/2019 tani 58,000; mwaka 2019/2020 tani 59,000 na mwaka 2020/2021 hadi kufikia tarehe 4/12/2020 uzalishaji ulikuwa ni tani 40,000 tu.
"Kama Wilaya tuna taarifa kuwa tuna wakulima 493 ambao wana hekta 481 ambazo zinahitaji miche mipya ya mikorosho. Chuo cha Naliendele wanayo miche, lakini pia Newala tunavyo vitalu vya miche, kwa hiyo tuhakikishe kuwa tunapanda miche mipya kwa kuwa inapatikana kwa wingi." Amesema Mhe. Mangosongo.
Akiwa kwenye mkutano huo, Mhe. Mangosongo aliwaruhusu wakulima kueleza changamoto wanazokutana nazo kwenye kilimo ili wataalamu wazifanyie kazi na kuleta tija na ongezeko kwenye uzalishaji wa mazao ya kilimo.
Wakizungumza kwa nafasi tofauti, wakulima waliohudhuria mkutano huo walieleza changamoto zinazowakabili kwenye kilimo cha korosho kuwa ni pembejeo kutopatikana kwa muda muafaka; mikorosho kukumbwa na magonjwa mbalimbali yakiwemo majani ya mikoroso kujikunja, korosho kubadilika rangi na kuwa kama zimeungua na majani machanga kujikunja na kuwa na ukungu.
Pia wakulima walieleza changamoto ya majani ya mikorosho na maua kupukutika mara baada ya kupulizia dawa ya unga kwenye mikorosho; baadhi ya mikorosho kutochipusha maua, mikorosho kutozalisha kwa wingi baada ya kubadili pembejeo toka ya unga kwenda ya maji hivyo wataalamu wachunguze kama dawa zimeisha muda wake au la na mashamba ya mikorosho kuvamiwa na wadudu aina ya sangala.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI Naliendele) akitoa maelekezo ya kitaalam kwa viongozi na wakulima waliohudhuria mkutano katika uzinduzi wa kampeni ya kuondoa mapori na kuongeza uzalishaji.
Akijibu maswali na changamoto za wakulima hao, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI - Naliendele) Dkt. Fortunatus Kapinga alisema kuwa kuna sababu mbalimbali zinazosababisha changamoto hizo hivyo kuwasisitiza wakulima kuwa na matumizi sahihi ya dawa zilizopendekezwa na wataalam na kupulizia dawa kwa muda unaotakiwa na kipimo kilichoainishwa; kupanda mbegu bora ambazo zinaweza kupambana na magonjwa; kutopanda dawa kwenye mikorosho kama hakuna dalili yoyote ya ugonjwa; mikorosho iliyozeeka inasababisha kupunguza uzalishaji hivyo iondolewe na ipandwe mipya au ikatwe ili ichipue upya; mikorosho ipandwe kwa nafasi kulingana na ukubwa wa shamba (miche 27 kwa ekari moja) na shamba muda wote kuwa safi ili kutovutia wadudu na kupulizia dawa ya kuua wadudu kwenye makazi ya wadudu hao.
Aidha katika kampeni hiyo ya kuondoa mapori na kuongeza uzalishaji, Mhe. Byakanwa ameagiza kuyafufua mashamba yote yaliyotelekezwa kwa kuyafanyia usafi na kupanda mazao, na baada ya tarehe 31 Januari 2021 mashamba yatakayobainika kuendelea kutelekezwa wamikiki watapigwa faini au kupokonywa na mashamba hayo kumilikishwa Halmashauri; pia vijana wamepigwa marufuku kukaa vijiweni na kuzurura muda wa kazi ma endapo watabainika kufanya hivyo watakamatwa na kupewa adhabu ya kwenda kulima mashamba ya Halmashauri. Aidha viongozi wote wa Chama kikuu cha ushirika (TANECU) na vyama vya msingi (AMCOS) wametakiwa kuwa na mashamba ambayo wakulima watayatumia kujifunza.
Kampeni hii ya kuondoa mashamba pori na kuongeza uzalishaji imelenga kuondoa mashamba pori yote, kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali ikiwemo korosho.
Akifunga mkutano huo, Mhe. Mangosongo amewataka wananchi kuilinda amani ya nchi kwa kutoa taarifa za wageni wote wanaofika katika maeneo yao kutoka nje ya Wilaya ya Newala ili wageni hao waandikwe kwenye daftari la wageni la kijijo kwa lengo la kutambuana na kudumisha ulinzi na usalama wa raia.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Newala Mhe. Aziza Mangosongo, wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Newala, Meneja wa TANECU, Mkurugenzi wa TARI Naliendele, Mbunge wa Newala vijijini Mhe. Maimuna Mtanda, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Mhe. Ladda Mfaume Tamimu, waheshimiwa madiwani, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Duncan Thebas, wakuu wa idara na vitengo wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala, wakulima na waandishi wa habari.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa