Katika utekelezaji wa Utawala bora, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Newala shilingi bilioni mbili na milioni mia mbili na kumi (Tsh. 2,210,000,000).
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Duncan Thebas akitoa taarifa kwenye mkutano wa baraza la madiwani uliofanyika jana tarehe 04/05/2021 katika ukumbi wa chuo cha ualimu Kitangari.
Akizungumza katika mkutano wa baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala wa kujadili utekekelezaji wa shughuli za maendeleo za kipindi cha robo ya tatu (Januari mpaka Machi) kwa mwaka wa fedha 2020/2021, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Duncan Thebas ameeleza kuwa Halmashauri imepokea fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa jengo la ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Newala; Ununuzi wa gari la Mkurugenzi Mtendaji na uendelezaji wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya.
“Halmashauri ya Wilaya ya Newala imepokea kiasi cha shilingi bilioni moja kutoka Serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa jengo la ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Newala, pia tumepokea fedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango shilingi milioni mia mbili na kumi kwa ajili ya ununuzi wa gari la Mkurugenzi Mtendaji likiwa ni ombi maalum, na tumepokea bilioni moja kutoka Serikali kuu ikiwa ni awamu ya pili kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya kwa kuongeza majengo matano ambayo ni stoo ya dawa, jengo la utawala, jengo la vipimo vya mionzi, jengo la kufulia nguo na jengo la wazazi, ambapo awali tulishapokea milioni mia tano zilizotumika kujenga majengo ya mapokezi ya wagonjwa wa nje (OPD) na maabara.” Alisema Bw. Thebas
Itakumbukwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Newala ni moja ya Halmashauri 31 zilizotakiwa kuhamia katika maeneo yao ya Utawala mwaka 2019, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa awamu ya tano, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, hivyo ujenzi wa jengo la ofisi ya Halmashauri ya Wilaya utapelekea watumishi kupata mazingira bora ya kufanyia kazi, kuwahudumia wananchi katika sehemu moja hivyo kuwezesha upatikanaji wa huduma bora na kutekeleza dhana ya utawala bora kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Mbunge wa jimbo la Newala Vijijini Mhe. Maimuna Mtanda akitoa ufafanuzi juu ya fedha za mfuko wa jimbo katika mkutano wa baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Kwa wakati mwingine Mbunge wa jimbo la Newala Vijijini, Mhe. Maimuna Mtanda ametumia nafasi hiyo kueleza ujio wa fedha za mfuko wa jimbo kwa mwaka huu 2021 na namna zinavyotumika.
“Fedha za mfuko wa jimbo tulizopokea ni milioni arobaini na moja, laki moja na elfu thelathini na tano. Fedha hizo zimetumika kutimiza maombi ya wananchi kwa Mbunge. Kwa kuanzia tumenunua simenti na mabati na vitagawiwa kwa vijiji vilivyotuma maombi hayo, na wale ambao hawatapata kwa awamu hii wawe wavumilivu watapata kwa awamu nyingine kwa kuwa maombi ni mengi kuliko fedha tulizopokea.” alisema Mhe. Mtanda.
Mkutano huo wa baraza la madiwani umefanyika jana tarehe 05/05/2021 katika ukumbi wa chuo cha ualimu Kitangari, ambapo pamoja na mambo mengine, wajumbe walijadili taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyopo kwenye Halmashauri, ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri, kupitisha kibali kilichotolewa na Serikali kuwapandisha vyeo watumishi 367 na kuwabadilisha kada watumishi 38 waliotengewa bajeti na ikama kwa mwaka wa fedha 2018/2019, 2019/2020 na 2020/2021.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa