Halmashauri ya Wilaya ya Newala imefanya maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji wa mtoto siku ya Jumanne tarehe 06/08/2019 katika kijiji cha Tuyangatane, kata ya Malatu kwa kuwakumbusha wakazi wa Newala faida za unyonyeshaji.
Akihutubia katika maadhimisho hayo mgeni rasmi ambaye ni kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bi. Magreth Lokonda aliwashukuru shirika la Hellen Keller International kwa kufanikisha maadhimisho hayo, pia alitumia nafasi hiyo kusisitiza umuhimu wa mama aliyejifungua kuanza kumnyonyesha mtoto ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa.
Bi. Likonda alieleza kuwa unyonyeshaji wa mtoto ni muhimu kwa kuwa maziwa ya mama yanamsaidia mtoto kukua vizuri kimwili na kiakili, kumkinga na magonjwa hasa yale ya mfumo wa hewa, mama kupunguza uzito uliopatikana kipindi cha ujauzito na pia unyonyeshaji hutumika kama njia ya asili ya uzazi wa mpango..
Aidha, baba wa watoto na wana familia kwa ujumla wamehimizwa kumsaidia mama kufanya shughuli za nyumbani ili mama apate muda wa kula vizuri, kupumzika na kumnyonyesha mtoto kwa wakati.
Wakati huo huo, Mratibu wa mradi wa Amka kutoka shirika la Hellen Keller International Bw. Juma Mziwanda alieleza kuwa mradi huo wa Amka ‘rise for nutrition’ umewasaidia wakina mama kupata elimu hivyo kuwa na muamko mkubwa wakuwapatia watoto maziwa ya mama tu miezi sita ya mwanzo baada ya kuzaliwa na hivyo kupelekea afya za watoto kuwa nzuri na maradhi ya watoto chini ya miezi sita kupungua. Bw. Mziwanda alisisitiza kuwa mafanikio ya mtoto kimwili na kiakili yanajengwa ndani ya siku 1000 tangu kutungwa kwa mimba.
Aidha, Mratibu wa lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bi. Somoe Bakari alieleza kuwa malengo ya maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji duniani kwa mwaka 2019 ni kuinua uelewa wa jamii kuhusu namna usawa wa kijinsia, sheria na kanuni zinavyoweza kulinda, kuendeleza na kusaidia unyonyeshaji maziwa ya mama na hivyo kuboresha lishe ya watoto.
Maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji kwa watoto kitaifa na kimataifa hufanyika kuanzia tarehe 1 mpaka 7 ya mwezi wa nane kila mwaka. Na kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu 2019 ni ‘Wawezeshe wazazi kufanikisha unyonyeshaji’
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa