Mkutano wa baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala wapitisha makadirio ya bajeti ya shilingi bilioni kumi na saba, milioni mia tatu ishirini na nane na elfu tisini na tano (17,328,095,000.00).
Akiwasilisha kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala, Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Juma Rahisi ameeleza kuwa, kwa mwaka wa fedha 2019/2020, Halmashauri kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwemo ruzuku kutoka Serikali kuu, wahisani wa maendeleo na mapato ya ndani ya Halmashauri imekadiria kukusanya jumla ya shilingi 17,328,095,000.00 ambayo itatumika katika kuhudumia sehemu kuu tatu ambazo ni mishahara ya watumishi, matumizi ya kawaida ya uendeshaji wa ofisi za Halmashauri na kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Bw. Rahisi alieleza kuwa mapato kutoka Serikali kuu yanakadiriwa kuwa kiasi cha shilingi 15,519,796,000.00, wahisani wa miradi ya maendeleo shilingi 375,679,000.00 na mapato ya ndani shilingi 1,432,620,000.00.
Halmashauri ya Wilaya ya Newala kwa vyanzo vyake vya ndani imekadiria kukusanya mapato yenye thamani ya shilingi 1,073,800,000.00 kutoka vyanzo vya mapato halisi na shilingi 358,820,000.00 kutoka vyanzo vya mapato lindwa ambavyo ni mfuko wa elimu, ada ya wanafunzi kidato cha 5 na cha 6, gharama za mfuko wa afya ya jamii, bima ya afya, malipo ya papo kwa papo na mfuko endelevu wa dawa (DRF).
Makadirio hayo ya makusanyo ya mapato ya ndani ni pungufu ya shilingi 489,647,000.00 ya makadirio ya bajeti ya mwaka 2018/2019 ambayo ilikuwa ni shilingi 1,922,267,000.00 sawa na upungufu wa asilimia 34.
Akiendelea kuzungumza kwenye baraza hilo la madiwani, Bw. Rahisi alifafanua kuwa kuna sababu mbalimbali zilizopelekea kushuka kwa makisio ya mapato ya ndani kwa mwaka 2019/2020 ambazo ni kukosekana kwa masoko ya mazao mchanyanyiko, uwepo wa makadirio makubwa kwa baadhi ya vyanzo kuliko hali halisi ya makusanyo, kuyumba kwa makusanyo yatokanayo na mfuko wa elimu na kubadilika kwa mfumo wa ununuzi wa korosho.
Mkuu wa Wilaya ya Newala Bi. Aziza Mangosongo (aliyesimama) akizungumza kwenye mkutano wa baraza la madiwani la kupitia rasimu ya bajeti ya Halmashauri ya mwaka 2019/2020
Akizungumza katika baraza hilo, Mkuu wa Wilaya ya Newala, Bi. Aziza Mangosongo, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Newala kwa kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato ambapo kwa sasa imeanzisha kituo kikubwa cha mabasi katika eneo la kitangari ambapo mabasi yote yanayofanya shughuli za usafirishaji wa abiria na yanayopita katika eneo la kitangari yanatakiwa kuingia, kupakia na kushusha abiria katika kituo hicho na kulipa ushuru hivyo kuipatia mapato Halmashauri.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Mussa M. Chimae (aliyesimama) akitolea ufafanuzi hoja zilizoibuliwa kwenye mkutano wa baraza la madiwani la kupitia rasimu ya bajeti ya Halmashauri ya mwaka 2019/2020
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Bw. Mussa Chimae, amewaeleza wajumbe wa baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Newala kuwa Halmashauri kwa sasa imedhamiria kuongeza zaidi mapato kwa kuibua vyanzo vipya vya mapato na kuboresha vyanzo vya zamani. Na hili linajidhihirisha kwenye uanzishwaji wa kituo kikubwa cha mabasi katika eneo la kitangari, ujenzi wa mabanda ya biashara kuzunguka kituo hicho, uanzishwaji wa kituo cha kupimia na kuuzia korosho zilizobanguliwa eneo la Kitangari ambapo Halmashauri inapata ushuru kwenye biashara hiyo na uimarishwaji wa kituo cha redio Newala ambacho ni mali ya Halmashauri ili kuongeza wigo wa usikivu, kuboresha miundombinu na maslahi ya watumishi na kuvutia wateja mbalimbali kutangaza na redio Newala hivyo kuongeza mapato ya ndani yaHalmashauri.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Mhe. Chitwanga Ndembo (aliyesimama) akifunga mkutano wa baraza la madiwani la kupitia rasimu ya bajeti ya Halmashauri ya mwaka 2019/2020
Akifunga mkutano huo wa baraza la Madiwani, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Mhe. Chitwanga Ndembo amewataka timu ya menejimenti ya Halmashauri kuyafanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa kwenye makadirio ya bajeti ya Halmashauri kwa mwaka 2019/2020 ili kuboresha huduma kwa wananchi na maslahi ya waheshimiwa madiwani hivyo kuleta heshima kwa viongozi hao.
Newala
Anuani ya Posta: P.O. Box 16
Simu: +255232410251
Mobile:
Barua pepe: ded@newaladc.go.tz
Hakimiliki@2016 Halmashauri ya Wilaya ya Newala. Haki zote zimehifadhiwa